MAONESHO YA MUHARRAM EXPO 2025 YAZINDULIWA KWA MBWEMBWE MNAZI MMOJA

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Maelfu ya wananchi wanatarajiwa kunufaika na huduma mbalimbali katika Maonesho ya Pili ya Huduma za Kifedha na Kijamii – Muharram Expo 2025, yaliyozinduliwa rasmi leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo yanafanyika sambamba na kuanza kwa mwaka mpya wa Kiislamu 1447 Hijria, yakibeba kaulimbiu isemayo: “Onesha Kujali Jamii, Toa Huduma, Sambaza Amani.”

Tukio hilo limelenga kuelimisha na kuwapatia wananchi huduma bunifu zisizo na riba, zenye kuzingatia misingi ya Shari’ah, pamoja na huduma muhimu katika nyanja za afya, elimu, na sheria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, mwakilishi wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU), Sheik Mohammed Issa, alisema maonesho hayo yanatoa jukwaa la kipekee kwa jamii kujifunza mbadala wa huduma za kifedha zilizo rafiki kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

“Tunatoa elimu kuhusu VICOBA, SACCOS, mifuko ya uwekezaji halal, hatifungani zisizo na riba (Sukuk), na hisa halali. Lengo letu ni kuwajengea wananchi uwezo wa kifedha bila kwenda kinyume na imani zao,” alieleza.

Zaidi ya huduma za kifedha, wananchi pia wanapata huduma za afya ikiwemo uchunguzi wa magonjwa, uchangiaji damu salama, huduma za wakfu, na msaada wa kisheria kutoka kwa wanasheria waliobobea katika fani mbalimbali.

Kwa ajili ya usalama wa kiafya wa wageni wote, waandaaji wameweka gari la wagonjwa (ambulance) maalum kwa ajili ya dharura zitakazojitokeza katika eneo la maonesho.

Aidha, wananchi wanapewa fursa ya kujiunga na elimu ya juu kupitia mfumo wa Chuo Kikuu Mtandaoni (Online University) pamoja na kununua vitabu mbalimbali vinavyohusu masuala ya dini, jamii, na uchumi.

Kwa mujibu wa ratiba, maonesho hayo yatadumu kwa siku saba kuanzia Julai 18 hadi Julai 24, 2025 na yataambatana na mihadhara pamoja na semina kutoka kwa wataalamu wa fani mbalimbali, watakaogusia mada kama: Madhara ya Riba, Huduma za Bima Halal, Fursa za Uwekezaji wa Kiislamu, Umuhimu wa kuweka mali katika Wakfu

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo.

BARAZA KUU limetoa shukrani kwa wadhamini na taasisi zote zilizoshiriki kufanikisha tukio hilo muhimu, zikiwemo CIFCA, Yusra Sukuk, Yusra Takaful, JAI, TAMPRO, YEMCO, Awqaf Tanzania, Benki ya KCB Sahl, Amana Bank, pamoja na wataalamu waliotoa huduma kwa moyo wa kujitolea.


Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi